Azam FC VS URA fainali ya Mapinduzi Cup 2018….


Mabingwa watetezi wa kombe la Mapinduzi , Azam FC wameonyesha nia ya kulitetea  kombe hilo baada ya kuitungua klabu ya Singida United goli 1 – 0 katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa katika dimba la Amaan , visiwani Zanzibar .

Goli pekee la Azam FC lilifungwa na mshambuliaji Shaaban Idd dakika ya 78 baada ya kutumia vema mpira wa kurushwa wa Bruce Kangwa, kabla ya kuupokea na kuwazidi maarifa mabeki wa Singida United na kupiga shuti safi la juu lililomshinda kipa Peter Manyika.

Hiyo ni fainali ya pili mfululizo kwa mabingwa hao watetezi wa michuano hiyo baada ya mwaka jana kutinga fainali na kuichapa Simba bao 1-0, lililofungwa na nahodha Himid Mao ‘Ninja’.

Kwa matokeo hayo, Azam FC itakutana na URA ya Uganda kwenye mechi ya fainali itakayofanyika Januari 13 mwaka huu katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Mechi hiyo itakumbushia mchezo wa Kundi A ambao ulihusisha timu hizo na Azam FC kupoteza kwa bao 1-0, lililofungwa na Nicholas Kagaba, hiyo inamaanisha kuwa timu bora za michuano hiyo zilizoingia fainali zimetoka kundi hilo.

Mabadiliko yaliyoibeba Azam FC hadi kushinda fainali hiyo yalikuwa ni ya kuwaingiza viungo Frank Domayo, winga Idd Kipagwile, na yale ya dakika za mwisho yaliyozaa bao ya Shaaban na kiungo mkabaji Braison Raphael.

Azam FC inaingia fainali baada ya kucheza mechi tano, nne za makundi ikishinda tatu dhidi ya Mwenge (2-0), Jamhuri (4-0) na Simba (1-0) ikipoteza mmoja dhidi ya URA (1-0) kabla ya nusu fainali kuichapa Singida United.

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com