Duh! Eti yanga hawajui Niyonzima alipo….


KOCHA wa Yanga, Hans Pluijm amesema amekasirishwa na kitendo cha mchezaji wake Haruna Niyonzima kuchelewa kuungana na wenzake kwa ajili ya michezo ya ligi huku akishindwa kabisa kutoa sababu zilizomfanya kuchelewa huko.

Niyonzima ndiye mchezaji pekee wa Yanga, ambaye hajawasili hadi sasa kuungana na wenzake, akidaiwa kuzima simu zake pasipokutoa taarifa kwa kocha wala uongozi wake.

Nae Jerry Muro alipoulizwa kuhusu swala lake alisema hivi , ” Wanachama wa Yanga waelewe kwamba Niyonzima hatupo nae. Niyonzima ana matatizo yake na uongozi ukitaka kujua hilo ongea na Tibohola mimi sijui chochote.”

Akiendelea kueleza hasira zake , Kocha wa Yanga, Hans Pluijm alisema amechoshwa na kitendo hicho ambacho sio mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kufanya, ni tatizo ambalo amekuwa akilirudia mara kwa mara anapopewa ruhusa kwenda kwao Rwanda.

Haruna-Niyonzima-Yanga-Bongosoka

“Nimechoshwa na Niyonzima. Nikimpigia simu kujua tatizo na kutuma meseji hajibu kabisa,” alisema. Pluijm alisema mchezaji huyo ambaye alikuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa, wakati anaondoka alionywa kuwa asichelewe kama ambavyo amekuwa akifanya siku za nyuma, lakini hajabadilika.

Alisema kitendo cha kuchelewa kwake, ni sawa na kuvunja sheria na kanuni za klabu na pia amewaangusha wachezaji wenzake, timu na hata wadau wa Yanga wanaompenda. “Niyonzima ameshindwa kuheshimu majukumu yake kama mchezaji wa kulipwa na hii sio mara ya kwanza, tuliwahi kukaa naye na kujadili kabla ya kwenda katika timu ya Taifa, tulimshauri na kumuonya,”alisema.

Wachezaji wote wa Yanga waliokuwa wanazitumikia timu zao za Taifa katika michezo ya Chalenji wamewasili na wengine walionekana wakicheza katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mgambo mkoani Tanga.

Alipoulizwa jana kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alisema watamchukulia hatua za nidhamu kiungo huyo. Kama alivyosema Pluijm, pia Katibu Mkuu huyo wa Yanga amesema kiungo huyo amekuwa na kawaida ya kuchelewa kurudi anapopewa ruhusa ya kurejea nchini kwao.

“Iwapo angecheza kwenye mchezo wa jana (juzi) dhidi ya Mgambo pengine tusingetoa hiyo sare ambapo huenda angesaidia kuleta matokeo mazuri kutokana na umuhimu wake kikosi cha kwanza,” alisema Katibu huyo. Wakati huohuo, Pluijm amezungumzia mchezo wa kesho dhidi ya African Sports kuwa wamejipanga na lazima washinde.

Alisema katika mchezo huo wanategemea kuwepo na baadhi ya wachezaji waliokosekana dhidi ya Mgambo kama Nadir Haroub na Donald Ngoma waliokuwa majeruhi ambao kwa sasa wanaendelea vizuri.

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com