Lwandamina: Muacheni Pluijm afanye kazi..


Kocha  wa Yanga, George Lwandamina, amesema hana tatizo na aliyekuwa kocha wa timu hiyo ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo, Hans van der Pluijm na kutaka Mholanzi huyo aachwe afanye kazi yake.

Akizungumza muda mfupi baada ya mazoezi ya timu hiyo visiwani Zanzibar, Lwandamina alisema amekuwa akipata ushirikiano mzuri kutoka kwa Pluijm na kwamba taarifa kuwa kocha huyo wa zamani anachangia timu kutofanya vizuri kutokana na ushawishi wake mkubwa kwa wachezaji wa timu hiyo si kweli.

“Nimesoma kwenye vyombo vya habari juu ya hilo la Pluijm, nafikiri wamwache afanye kazi yake, kila mtu anafanya kazi yake hapa na tumekuwa na ushirikiano mkubwa,” alisema Lwandamina.

Aidha, kocha huyo raia wa Zambia, alisema kwa sasa mawazo yao wameyaelekeza kwenye michuano ya Ligi Kuu ambayo kwa sasa imesimama kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

 

“Hicho ndicho kipaumbele cha kwanza, kuhakikisha timu inatetea ubingwa wake na hili linahitaji ushirikiano wa Wanayanga wote,” alisema Lwandamina.

Alisema pamoja na ugumu wa ligi, lakini hakuna wanachokifikiria zaidi ya namna ya kuipa ubingwa Yanga inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa nyuma kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya Simba inayoongoza ligi ikiwa na pointi 44.

Katika hatua nyingine, Lwandamina alisema michauno inayoendelea sasa ya Kombe la Mapinduzi ni sehemu ya kukiweka vizuri kikosi chake kwa ajili ya mechi za ligi zitakazoanza baadaye Januari 13, mwaka huu.

 

Yanga leo usiku inacheza mchezo wake wa pili wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Zimamoto baada ya juzi kuifumua Jamhuri kwa mabao 6-0.

Usisahau kujisajili kwenye mchezo mpya wa ligi kuu Tanzania bara | BONYEZA HAPA KUJIUNGA .Tufuate facebook , twitter na instagram .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , [email protected]