Shiza Kichuya: simba ni maneno zaidi ya vitendo kuhusu usajili wangu


KIUNGO wa Mtibwa Sugar, Shiza Kichuya, amesema anafikiria kubadili mawazo yake ya kujiunga na Simba ili kuendelea kuitumikia timu hiyo ambayo imemfanya kujulikana.

Baada ya kufanikiwa kuwanasa Mzamiru Yasini na Ibrahim Mohamed, Simba ipo katika harakati za kuinasa saini ya winga huyo aliyefanya vizuri msimu uliopita akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar.

Kichuya, alisema anataka kubadili mawazo baada ya kuona Simba wakisuasua mchakato wa usajili wake, hivyo ni vyema akabaki kuitumikia timu yake ambayo imemuibua na kumfanya aitwe hadi timu ya Taifa.

Shiza-Kichuya-Mtibwa-Sugar-bongosoka

“Kila siku nasikia Simba wamemsajili mchezaji huyu mara yule, wakati mimi ndiyo nilikuwa wa kwanza, lakini hadi sasa yamekuwa ni maneno hakuna vitendo, sasa pengine hawanihitaji na mimi nimeanza kughairi bora nibaki hapa ili kutoa mchango wangu kwa Mtibwa,” alisema.

Winga huyo alisema hana kinyongo na wachezaji ambao wamesajiliwa, ispokuwa anawashangaa viongozi wa Simba kwa kumuahidi mambo halafu wanashindwa kuyatekeleza na kumfanya yeye kutojielewa yupo upande gani.

Kichuya ndiye alikuwa mchezaji wa kwanza kutajwa kuwa angejiunga na Simba baada ya ligi kumalizika lakini hadi sasa mpango huo haujakamilika, huku tayari wachezaji wengine watano wakiwa wameshakamilisha usajili wao kuichezea Simba msimu ujao.

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com