Simba amla Yanga na kutinga fainali , kukutana na Azam FC…


Klabu ya wekundu wa msimbazi Simba , jana usiku iliweza kuibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao wa jadi , Yanga SC baada ya kuitungua kwa mikwaju ya penalti 4 – 2 katika mechi ya nusu fainali  kombe la Mapinduzi . Ushindi huo unaifanya Simba kushinda mara nne kati ya mara tano alizokutana na Yanga kwenye uwanja huo.

Watani hao wa jadi walikwenda kwenye mikwaju ya penalti baada ya mechi kuisha kwa sare ya bila kufungana katika dakika 90 za mchezo. Jonas Mkude alikuwa wa kwanza kupiga mkwaju wa penalti kwa timu yake ya Simba ambapo alipata kabla Kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Yanga kukosa mkwaju wake baada ya kipa wa Simba Daniel Agyei kupangua.

Agyei alipiga penalti ya pili kwa Simba ambapo alipata huku Method Mwanjali akikosa, Muzamiru Yassin na Bukungu walipata penalti zao na kwa upande wa Yanga Simon Msuva na Thabani Kamusoko walifunga huku Haji Mwinyi akikosa. Kwa ujumla mechi hiyo haikuwa na ufundi na ilitawaliwa na rafu za hapa na pale huku timu zikishambuliana kwa zamu katika kila kipindi.

Ni Simba ndio walionza kugongeana vizuri katika dakika ya saba lakini beki Kelvin Yondani akaokoa hatari hiyo. Dakika moja baadae Haruna Niyonzima alipata nafasi nzuri na kupiga shuti lililodakwa vizuri na kipa wa Simba Daniel Agyei.

Simon Msuva alikosa bao katika dakika 15 baada ya kuunganisha pasi ya Amisi Tambwe na dakika ya 36 Jamvier alikoa mpira uliokuwa ukielekea golini mwa Simba huku tayari kipa Agyei akiwa ‘ameshapotea’.

Zikiwa zimesalia dakika mbili kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, Mohamed Ibrahim ‘Mo’ nusura aifungie Simba bao lakini mpira aliopiga uligonga mwamba wa juu na kumkuta Shiza Kichuya ambaye alipiga na mpira ukatoka nje. Kipindi cha pili kilianza kwa taratibu kama ilivyokuwa cha kwanza na wachezaji wa timu zote wakionekana kusubiri kwenda kwenye penalti.

Yanga imepata kipigo hicho baada ya kufungwa mabao 4-0 katika mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Azam. Kwa matokeo hayo, Simba sasa itacheza fainali za michuano hiyo dhidi ya Azam keshokutwa. Azam ilikuwa ya kwanza kutinga fainali baada ya kuifunga Taifa Jang’ombe bao 1-0 lililofungwa na Frank Domayo kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Jang’ombe Ahmed Ally katika dakika ya 33.

Usisahau kujisajili kwenye mchezo mpya wa ligi kuu Tanzania bara | BONYEZA HAPA KUJIUNGA .Tufuate facebook , twitter na instagram .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , [email protected]