Simba kuwavaa URA ya Uganda leo Mapinduzi Cup..


Klabu ya wekundu wa Msimbazi , Simba itashuka dimbani leo katika mchezo wa mwendelezo wa  michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya mabingwa watetezi timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA).

Simba inaingia uwanjani leo ikiwa imetoka kuinyuka KVZ bao 1-0  juzi usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Ushindi huo uliotokana na bao pekee la kiungo Muzamil Yassin dakika ya 43, umeifanya Simba ifikishe poinit sita katika Kundi A baada ya kucheza mechi mbili. Ni ushindi wa pili mfululizo kwa Simba katika michuano hiyo, baada ya kuilaza Taifa Jang’ombe 2-1 katika mechi yake ya kwanza .

Kocha msaidizi wa timu hiyo ,  Jackson Manyanja alisema kuwa mechi hiyo kwao wanaichukulia kama fainali kwa vile URA watataka kujenga heshima ya utetezi wa taji lao.

“URA michuano hii ni bingwa mtetezi, lakini kwenye Ligi ya Uganda ina shika nafasi ya sita, najua watataka kujionesha ni wakali wakati hawana lolote, sisi kwenye Ligi tunaongoza ni lazima tulinde heshima yetu na kuwaonesha kuwa sisi ni vinara kwenye msimamo wetu wa ligi”alisema Mayanja.

Alisema anasikitishwa na mashabiki wanaobeza ushindi wao kiduchu wanaopata katika michuano hiyo kwa kufunga bao moja kila mechi na kwamba kwao muhimu ni ushindi na si wingi wa magoli.

“Muhimu ni pointi tatu, ushinde mabao 10 mabao sita mwisho wa siku pointi ni zile zile tatu sawa na sisi tunaoshinda bao moja, tutaenda hivi lakini mwisho wa siku tutakuwa mabingwa, hivyo wasitubeze, wanaweza kufunga hata magoli 20, lakini mwisho wa siku wakatoka kappa, “alisema.

Hatahivyo, Mayanja alisema kuwa wafungaji wao wamekuwa wakiwaangusha licha ya kuwapa mbinu mbali mbali za ufungaji lakini wamekuwa hawazingatii na kufanya kupoteza magoli mengi ya wazi.

Iwapo Simba itashinda mchezo wa leo dhidi ya URA itakuwa imekata tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali akimsubiri mshindi wa pili wa Kundi B kusaka nafasi ya kucheza fainali.

Usisahau kujisajili kwenye mchezo mpya wa ligi kuu Tanzania bara | BONYEZA HAPA KUJIUNGA .Tufuate facebook , twitter na instagram .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , [email protected]