Simba VS Yanga hakuna mbabe…


Mchezo wa watani wa jadi kati ya  Simba  na Yanga umemalizika huku timu hizo zikitoshana nguvu kwa kuvungana goli 1 – 1 katika mchezo wa raundi ya 8 ligi kuu Tanzania bara uliopigwa  majira ya 10:00 jioni katika uwanja wa uhuru jijini Dar-es-salaam .

Shiza Kichuya ndiye aliyekuwa wa kwanza kutikisa nyavu za Yanga dakika ya 57 kabla ya Obrey Chirwa kuisawazishia timu yake dakika ya 60.

Kichuya amekuwa na bahati ya kuifungia timu yake inapokutana na Yanga ambapo sasa ameifunga Yanga mara tatu katika mechi alizocheza huku Chirwa ikiwa ni mara yake ya kwanza. Shiza alifunga bao hilo baada ya Okwi kupiga shuti ambalo kipa wa Yanga Youthe Rostand alilipangua na mpira kumkuta Kichuya aliyeachia shuti kali na kutikisa nyavu hizo huku Chirwa naye akijibu mapigo baada ya kupokea pasi ya Geofrey Mwashiuya dakika tatu baadae.

Wachezaji wanaotajwa sana kwa sasa na mashabiki wa soka hapa nchini kutokana na kasi yao ya ufungaji, Ajib wa Yanga na Emmanuel Okwi wa Simba walidhibitiwa vilivyo na mabeki wa timu zote mbili hivyo kushindwa kupachika bao katika mchezo huo.

Katika kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa kuviziana kama vile kila mmoja alikuwa anamsoma mwenzake tofauti na kipindi cha pili ambacho timu hizo zilionyesha upinzani mkubwa na mashambulizi ya mara kwa mara.

Makocha wote wawili waliamua kufanya mabadiliko kipindi cha pili ikiwa ni lengo la kupata matokeo mazuri zaidi ambapo kocha George Lwandamina aliwatoa Mwashiuya na Raphael Daudi nafasi zao zikichukuliwa na Emmanuel Martin na Pato Ngonyani.

Upande wa Simba, kocha Joseph Omog aliwatoa Laudit Mavugo, James Kotei na Mzamiru Yassin ambao nafasi zao zilichukuliwa na John Bocco, Jonas Mkude na Said Ndemla.

Katika mchezo huo mwamuzi Elly Sasii alitoa kadi za njano kwa wachezaji Kichuya kwa kosa la kwenda kwa mashabiki baada ya kuifungia bao timu yake pamoja na Ajibu aliyeonyesha utovu wa nidhamu kwa kubishana na refa baada ya kucheza rafu.

Baad ya ushindi huo makocha wapande zote mbili walipata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari.

Kocha msaidizi wa klabu ya Yanga Shadrack Nsajigwa amesema “Mchezo ulikuwa mgumu kwa kuwa timu zote zilijiandaa kwaajili ya kupata matokeo ya ushindi.”Amesema Nsajigwa.

Nsajigwa ameongeza “Nawapongeza sana wapinzani wangu kwakuwa ni timu nzuri ila nivigumu sana kubashiri nani angekuwa nyota wa mchezo naamini anaweza kutoka upande wowote.”

Kwa upande wa Kocha wa Simba SC, Joseph Omog amesema ” Ulikuwa mchezo mzuri,mgumu na ushindani tulipata nafasi nyingi lakini hatukuzitumia.”

Hata hivyo Omog alipoulizwa na waandishi juu ya safu yake ya ulinzi kupwaya na hata upande wa ushambuliaji kushindwa kufunga mabao kama ilivyozoeleka amesema ni kutokana na mchezo wenye.

Kwa matokeo hayo, Simba itakuwa kileleni kwa pointi 16 sawa na Yanga huku wekundu hao wakibebwa na tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com