Simba yaaga mashindano ya kombe la mapinduzi….


Klabu ya Wekundu wa msimbazi , Simba imeaga rasmi mbio za kuwania ubingwa wa kombe la mapinduzi baada ya kutunguliwa goli 1 – 0 na klabu ya URA ya Uganda katika mchezo wa mwisho wa kundi A .

Baada ya kufungwa goli 1 – 0 na Azam FC katika mchezo uliopita , Simba iliingia uwanjani leo ikijua wazi ni lazima iondoke na ushindi ili kuweza kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hii . Bao la pekee la mchezo lilitupiwa wavuni na mshambuliaji wa URA , Deboss Kalama baada ya ukosefu wa umakini wa mabeki wa Simba uliomuacha mfungaji huo nafasi ya kuachia shuti kali lililozama moja kwa moja golini .

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani, Simba ilifanya mashambilizi ya mara kwa mara kupitia kwa John Bocco ‘Adebayor dakika 30 na lile la dakika ya 75 la piga nikupige kati ya Bocco, Asante Kwasi na Ibrahim Mohamed ‘Mo’ mpira ukatoka nje.

URA inapanda kileleni mwa Kundi A ikifikisha pointi 10 baada ya kushinda mechi tatu na sare moja, wakati Azam FC iliyoshinda mechi tatu na kufungwa moja inamaliza nafasi ya pili.

Kwa matokeo hayo, Simba itawabidi watazame  maandalizi ya mashindano mengine ya ligi kuu pamoja na Kombe la Shirikisho.

Nusu fainali ya mashindano hayo, itachezwa kesho kutwa Jumatano na utaanza mchezo kati ya URA na Yanga saa 10:30 jioni na Azam itakipiga na Singida United saa  02:15 usiku katika uwanja huo huo wa Amaan.

 

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com