Simba yatwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara 2017/2018


Baada ya kukaa misimu minne bila kuchukua ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara, hatimaye klabu ya Simba imefanikiwa rasmi kuwa bingwa wa Ligi kuu Tanzania bara msimu wa mwaka 2017/2018.

Ubingwa wa Simba unakuja  baada ya timu ya Prisons kuifunga Yanga magoli 2-0 katika mchezo wa mwendelezo wa ligi kuu Tanzania bara na kuifanya Simba kuwa na  alama ambazo haziwezi kufikishwa na timu yoyote kwa sasa.

Katika mchezo wa leo mabao ya Tanzania Prisons yamefungwa na Eliuter Mpepo kwa penalti dakika ya 58 baada ya kiungo Mzimbabwe, ThabaniKamusoko kuushika mpira kwenye boksi na Salum Bosco aliyefunga la pili dakika ya 85 akitumia udhaifu wa mabeki wa Yanga.

Matokeo haya pia yanamaanisha Yanga SC hawatashiriki michuano ya Afrika mwakani, kwani tayari wametolewa pia na kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation (ASFC) katika hatua ya Robo Fainali tu.

Yanga imebakiza michezo mitano (5) mpaka sasa hivi ikiwa na alama 48 katika nafasi ya tatu.

Kama Yanga ikifanikiwa kushinda michezo yote hiyo mitano itakuwa imechukua alama 15 , alama ambazo ukiziongeza na alama 48 anakuwa na alama 63 ambapo itakuwa pungufu ya alama mbili za Simba ambayo ina alama 65 mpaka sasa ikiwa imecheza michezo 27.

Azam Fc inayoshika nafasi ya 2 na alama 49 haina uwezo pia ya kuzifikia alama za Simba kwa sababu wamebakiza michezo mitatu, ambapo wakishinda michezo hiyo mitatu watapata alama tisa ambazo ukiziongeza kwenye alama walizo nazo wanakuwa na alama 58.

Kwa hiyo Simba imekuwa bingwa rasmi wa ligi kuu Tanzania bara wakiwa wanasubiri wakisubiri mechi ya Singida United.

Mechi hii itakuwa ya kumamilisha ratiba tu na kulinda heshima kwa sababu Simba inataka kumaliza ligi ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja.

Yanga inauachia ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kukaa nao kwa misimu mitatu mfululizio wakati, Simba SC inatwaa taji la kwanza la ligi hiyo tangu mwaka 2012 walipochukua kwa mara ya mwisho.

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com