Simon Msuva naye ajifunga Yanga mpaka 2018


Uongozi wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Yanga, jana umemuongeza mkataba mpya mshambuliaji wake tegemeo, Simon Msuva, imeelezwa jijini Dar es Salaam. Mkataba wa awali wa kiungo huyo ambaye alitua Yanga akitokea Moro United ya Morogoro, ulikuwa unamalizika Mei mwakani lakini sasa atakuwa mali ya Yanga hadi 2018. Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, alisema wameamua kumuongeza Msuva mkataba kutokana na umuhimu wake katika kikosi cha Yanga na wanaheshimu mchango wake alioutoa katika klabu hiyo kwenye  msimu wa Ligi Kuu Bara uliomalizika. “Ni kweli Msuva tumemuongezea mkataba mpya wa miaka miwili na hivyo maana yake atakuwa mali ya Yanga ya Dar es Salaam hadi mwishoni mwa msimu wa 2017/2018,” alisema Tiboroha.

Simon-Msuva-Yanga-bongosoka

Katibu huyo aliongeza kuwa, mshambuliaji huyo ni mmoja wa wachezaji ambao ni matunda ya Yanga na wanajivunia na kiwango chake anachokionyesha ndani ya uwanja na anapokuwa kwenye timu ya Taifa (Taifa Stars). “Yanga ya sasa ina ushindani wa namba kwa sababu kila nafasi ina wachezaji wenye uwezo zaidi ya wawili, lakini kwa Msuva bado hana wasiwasi na kuwekwa benchi,” aliongeza. Alisema kuwa wiki iliyopita walianza kuuboresha mkataba wa mshambuliaji wao kutoka Burundi, Amissi Tambwe na baadaye watafuata kwa kiungo wao, Salum Telela na mchezaji mwingine atakayekuwa amemvutia zaidi Kocha Mkuu, Hans van der Pluijm. “Ni jambo lililowazi kwamba Yanga iko vizuri na kila siku wachezaji wanapewa somo ili wafanye mazoezi na waache uzembe kwa sababu itawagharimu, tumejipanga kuhakikisha tunatetea ubingwa  wetu,”  Tiboroha aliongeza.  Alisema bado hawajafunga zoezi la usajili na wataendelea kufanya hivyo kulingana na mahitaji ya kocha wao. Kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi yake kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), timu hiyo itaanza kuwania ubingwa huo kwa kuikaribisha Gor Mahia ya Kenya ifikapo Julai 18 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com