Taifa Stars yaitungua Cape Verde 2 – 0 taifa….


Timu ya taifa ya Tanzania , Taifa Stars jioni ya leo imeweza kuibuka na ushindi wa goli 2 – 0 dhidi ya Cape verde kwenye mchezo wa marudiano wa kundi L   kufuzu kucheza michuano ya Mataifa Afrika (AFCON) 2019 nchini Cameroon mchezo uliopigwa katika  Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam .

Bao la kwanza la Taifa Stars lilifungwa  na  mshambuliaji wa Difaa El Jadida ya Morocco Simon Msuva .  dakika ya 29 baada ya kupokea  pasi ya Mshambuliaji wa GRC Genk Mbwana Samatta.

Kipindi cha kwanza dakika ya 22  pia kilishuhudia Mbwana Samatta akikosa penati  kwa kugongesha mwamba wa juu  baada ya beki  Ianique dos Santos Tavares  kumuangusha Msuva kwenye eneo la boksi.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika , Taifa Stars ilikua mbele kwa bao 1 – 0 . Kipindi cha Pili, Mbwana Samatta alifanikiwa kuifungia Stars goli la pili   akimalizia pasi ya Mudathiri Yahya .

Mabadiliko waliyoyafanya Taifa Stars katika mchezo wa leo ni pamoja na  kumtoa Abdi Banda na kumuingiza John Bocco huku  Mudathir nafasi yake ikichukuliwa na Feisal Toto .

Ushindi wa leo ambao ni  wa kwanza kwa Taifa Stars kwenye mashindano haya, unaifanya ipande hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili.

Uganda  ndio vinara wa kundi hili ikiwa na pointi  saba huku ikicheza mechi tatu, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   Mechi kati ya Uganda na Lesotho inaendelea wakati huu ambapo tayari Uganda wanaongoza kwa goli 2 – 0 hadi dakika ya 50 .

Kikosi cha Taifa Stars kilikuwa: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Aggrey Morris, Abdi Banda/John Bocco dk51, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Himid Mao, Mudathir Yahya/Feisal Salum dk58, Mbwana Samatta/Rashid Mandawa dk89 na Simon Msuva.

Cape Verde: Graca Theirry, Almeid Tiago/Rocha Nuno dk64, Rodrigues Carlos, Barros Admilson, Tavares Ianique, Fortes Jeffry, Macedo Elvis, Rodrigues Garry, Soares Luis/Heldon Ramos dk53, Semed Jorge na Gomes Ricardo/Gilson Silva dk77.

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com