TFF waingilia kati sakata la Yanga kumtema Haruna Niyonzima


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeitaka klabu ya Yanga kumalizana na kiungo wao, Haruna Niyonzima kwa mujibu wa sheria na kanuni za usajili na mikataba kabla ya wao kuingilia kati mgogoro wa kimkataba baina ya pande hizo mbili.
Yanga imevunja mkataba baina yao na Niyonzima kutokana na kile kinachodaiwa kuwa mchezaji huyo ni mtovu wa nidhamu baada ya kuvunja baadhi ya vipengele vilivyopo katika mkataba wake kwa kuondoka klabuni bila ruhusa, kuchelewa kuripoti kambini pamoja na kucheza mechi ambazo si rasmi.

Haruna-Niyonzima-Yanga-Bongosoka
Kitendo hicho kimekuja ikiwa ni miezi mitano tu tangu pande hizo mbili kuamua kuingia mkataba mpya wa miaka miwili kabla ya kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.


Licha ya kuvunjwa mkataba huo, Yanga imemtaka kiungo huyo wa kimataifa wa Rwanda kuilipa Dola za Marekani 71,175 (Sh milioni 151.95) kama fidia ya gharama ambazo walizitumia kumpa mkataba mpya.


Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Rais wa TFF, Jamal Malinzi, alisema kuwa ni vizuri mikataba baina ya timu na mchezaji ikaheshimiwa ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima ambayo mara nyingi huugharimu upande mmoja.


“Kikubwa Yanga wakae na mchezaji wao ili kuyamaliza, kama ni kuvunja mkataba basi kila upande uridhie na sio huku wanavunja kisha upande mwingine wanashtaki kupinga kitendo hicho.


“Sisi kama TFF tuna wajibu wa kuwalinda pande zote mbili, lakini kwanza tunatoa nafasi ya kuyamaliza wenyewe kabla ya sisi kubeba jukumu la kutafuta suluhu,” alisema.


Alisema ifike wakati timu na mchezaji kila mmoja atambue majukumu yake na kuyatekeleza kulingana na mkataba unavyomtaka ili kuepuka kuvunja mikataba kusiko na lazima au kwa lengo la kunufaisha upande mmoja.

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com