Yanga yaafa mashindano ya Mapinduzi Cup


Klabu ya Yanga imeyaaga mashindano ya kombe la Mapinduzi  baada ya kufungwa kwa mikwaju ya  penalti 5 – 4 na URA ya Uganda.

Yanga ambayo ilikuwa ikipewa nafasi ya kufanya kweli katika michuano hiyo kwa kufika fainali na ikiwezekana kitwaa ubingwa, imeishia hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani unguja dhidi ya wapinzani wao hao ambao pia waliiondoa Simba katika hatua ya makundi.

Hadi dakika za kawaida za mchezo zinakamilika matokeo yalikuwa suluhu ndipo ikabidi mchezo huo uamuliwe kwa kupigwa mikwaju ya penati.

Yanga ilipata penati nne huku wapinzani wao wakipata tano . Mzambia Obrey Chirwa ambaye ameungana na timu leo asubuhi na akaaminiwa kupewa nafasi ya kucheza kuanzia dakika ya 53 akichukua nafasi ya Pius Buswita, ndiye aliyekosa penalti hiyo, iliyowaondoa Yanga katika mashindano hayo .

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, kiungo wa Yanga, Said Juma ‘Makapu’ alichaguliwa kuwa mchezaji bora (Man Of The Match).

Kutokana na matokeo hayo, sasa URA imefanikiwa kufuzu hatua ya fainali ambayo itachezwa Jumamosi hii, ikisubiri matokeo ya Azam FC dhidi ya Singida United.

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com