Yanga yaitandika Mlandege 2 – 1 kombe la mapinduzi…


Yanga imeanza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mlandege katika mchezo wa kundi B, uliopigwa uwanja wa Amaan Zanzibar.

Ushindi wa Yanga umepunguza kasi ya Mlandege ambayo ndiyo vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi zao sita, na Yanga wanapanda hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi tatu mabao mawili ya kufunga.

Kiungo mshambuliaji Juma Mahadhi ndiyo amefunga mabao yote mawili katika dakika za 6 na 36, na kurekebisha makosa yake ambayo amekuwa akiyafanya hata kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza.


Mlandege ndiyo waliouanza kwa kasi mchezo huo na kufanya mashambulizi makali kwenye lango la Yanga lakini mabeki wa Yanga walisimama imara na kuondosha hatari hizo langoni mwao.

Yanga ilijikuta ikipata pigo sekunde ya 53, tangu kuanza kwa mchezo baada ya beki wa Yanga na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kugongwa kichwani na mshambuliaji wa Mlandege na kupoteza fahamu jambo lilisababisha benchi la timu hiyo kufanya mabadiliko yasiyo ya lazima kwa kumuingiza Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Yanga ilipata bao lake la kwanza dakika ya 6, mfungaji akiwa Mahadhi aliyemalizia mpira wa kichwa uliopigwa na Pius Buswita kufuatia krosi nzuri ya beki wa kulia Ramadhani Kessy..

Mahadhi aliiandikia Yanga bao la pili dakika ya 36, safari hii akipokea pasi ya Papy Shishimbi aliyeunganisha krosi ya Haji Mwinyi ambaye katika mchezo huo alionekana amepoa kuliko ilivyokuwa kawaida yake.

Pamoja na jitihada za timu ya Mlandege kupambana kutaka kusawazisha mabao hayo zilionekana kushindikana na kufanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa nyuma mwa mabao hayo mawili.

Kipindi cha pili Mlandege walikianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kufuatia machozi dakika ya 47 mgfungaji akiwa Omary Makame aliyepokea pasi nzuri ya Mohamed Abdallah.

Katika dakika ya 86 wachezaji Endrew Vicent wa Yanga na Omary Makame wa Mlandege walitolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia kutaka kupigana wanjani na baada ya tukio hilo mchezo uliendelea kwa timu zote kushambuliana.

Yanga ilifanya mabadiliko matatu kwa pamoja ambapo iliwatoa Daud, Tshishimbi na Mahadhi na nafasi zao kuchukuliwa na Emmanuel MartinSaid Bakari na Yohana Nkomola ambao kiasi fulani waliongeza presha kwa wapinzani wao Mlandege.

Hadi dakika 90 za mpambano huo zinakamilika Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mlandege

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com