Yanga yajibu mapigo , yaichapa Stand United 4 – 0….


Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara, Yanga wameendelea kuifukuzia Simba  kileleni baada ya kuibuka na ushindi wa Mabao 4-0 dhidi ya Stand United katika mchezo uliopigwa  katika uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga .

Yanga ndio walioanza kushambuliwa katika dakika ya kwanza tu ya mchezo lakini shuti la Hamad Kibopile wa Stand United likashinda kuipita mikono Mkameruni Youthe Rostand. Baada ya hapo Yanga walianza kuimarika na kumiliki mpira kwa kiwango kikubwa wakitumia ufundi wa Ibrahim Ajibu na Geofrey Mwashiuya.

Yanga walipata Bao baada ya jitihada zao kuzaa matunda katika dakika ya 24 baada ya Ibrahim Ajibu kupiga Faulo nzuri iliyozama moja kwa moja nyavuni.

Dakika sita baadae juhudi za Obrey Chirwa za kuwachambua wachezaji wa Stand United zilizaa matunda baada ya kutoa pasi nzuri kwa Ibrahim Ajibu aliyeweza kutupia bao la pili .

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa Stand United kutaka kupata bao la kwanza na pengine kusawazisha lakini mambo magumu. Dakika ya 52 Yanga SC walipata Bao la tatu kupitia kwa Kiungo Pius Buswita kufuatia kupokea pande la Mpira wa kona uliochongwa na Geoffrey Mwashiuya.

Makosa ya mlinda mlango Frank Muwonge katika dakika ya 68 kujaribu kuucheza Mpira wa krosi wa Pius Buswita yalimgharimu baada ya mpira huo kumpita na kumkuta Obrey Chirwa ambaye naye akazipasia nyavu na kuweka bao la Nne.

Hadi kipyenga cha mwamuzi cha mwamuzi Erick Onako kinapulizwa Yanga walitoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 4-0 . Ushindi wa leo  ni mkubwa zaidi kwa Yanga kuupata msimu huu hasa katika michezo ya ugenini.

 

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com