Yanga yapata mrithi wa Donald Ngoma , Mrisho Ngasa kurejea kundini..


kama  ulidhani kwamba akiondoka Donald Ngoma Yanga itahangaika, basi umekosea sana kwani klabu hiyo imenasa bonge la kifaa ambacho ni moto wa kuotea mbali.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara wako mbioni kumuuza Ngoma, kwa moja ya klabu za Misri ambapo klabu za Al Ahly na Zamalek zinachuana kumuwania.

Kutokana na hali hiyo Yanga imeanza harakati za kuziba pengo la Ngona na wako katika hatua nzuri ya kumsajili mshambuliaji Walter Musona kutoka klabu ya FC Platinum ya Zimbabwe, alikotokea Ngoma.

Musona ni moja ya washambuliaji hatari sana wanaosifiwa kwa uwezo wake wa kupachika mabao kwa namna mbalimbali na jinsi alivyo fundi katika kuwatungua makipa.

Makali ya straika huyo yalionekana hata hapa Tanzania mwaka jana alipokuja na FC Platinum kwani ndiye aliyefunga bao moja katika mchezo uliomalizika kwa Yanga kushinda mabao 5-1.

Walter-Musona-bongosoka-yanga

Musona aliihangaisha ngome ya Yanga katika mchezo huo na alionekana kama ni mshambuliaji aliyetimia kila idara kwani alikuwa na kasi, alipambana  vilivyo na alikuwa mwiba mchungu ya safu ya ulinzi ya Yanga iliyoongozwa na nahodha wake Nadhir Haroub ‘Cannavaro.’

Mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga, alisema kuwa kutokana na suala hilo sasa wameamua kumchukua Musona kuwa kama mrithi wa Ngoma iwapo mpango wake wa kwenda Misri utakamilika

“Yanga inamuhitaji Musona na imeanza harakati za kumnasa mchezaji huyo kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Ngoma ambaye kwa sasa anawania wa timu mbili za Misri,” alisema mtoa habari huyo.

Musona ambaye ni straika, ni miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wanawaniwa na Yanga kwa muda mrefu tangu msimu uliopita ambapo ilikuwa aje kuchukua nafasi ya kiungo mshambuliaji Mbrazil, Andrew Coutinho lakini mipango haikukaa sawa.

“Kwa sasa Musona anaweza kutua nchini wakati wowote na mpango uliotumika kumsajili Ngoma na Kamusoko ndio huo huo unaotumika kumleta mchezaji huyu,” alisema kiongozi huyo.

Katika hatua nyingine uongozi wa Yanga unafanya mazungumzo na klabu ya Free State ya Afrika Kusini kwa ajili ya kumrejesha winga wake Mrisho Ngassa.

Ngassa ambaye aliondoka Yanga baada ya kumalika kwa msimu wa mwaka 2014/15 na kusajiliwa na timu hiyo kwa mkataba wa miaka minne ambapo hadi sasa ameshacheza msimu mmoja ndani ya timu hiyo.

Ngassa ambaye alikuwepo nchini na kuishuhudia Yanga ikicheza na Azama FC na kutwaa kombe la Shirikisho hivi karibuni, alisema yupo tayari kurejea Tanzania lakini hakuweka wazi atajiunga na timu gani.

Tufuate instagram , facebook na twitter .Unaweza pia kutuma stori yako ya michezo na sisi kuiweka kwa kubonyeza HAPA . Pia kutangaza nasi tutumie email , bongosoka@gmail.com